John 18:28-38

Yesu Apelekwa Kwa Pilato

(Mathayo 27:1-2, 11-14; Marko 15:1-5; Luka 23:1-5)

28 aNdipo Wayahudi wakamchukua Yesu kutoka kwa Kayafa na kumpeleka kwenye jumba la kifalme la mtawala wa Kirumi.
Jumba la mfalme la mtawala wa Kirumi lilikuwa linaitwa Praitorio.
Wakati huo ilikuwa ni alfajiri, ili kuepuka kuwa najisi kwa taratibu za ibada, Wayahudi hawakuingia ndani kwa sababu ya sheria za Kiyahudi. Wangehesabiwa kuwa najisi kama wangeingia nyumbani mwa mtu asiye Myahudi na wasingeruhusiwa kushiriki katika Sikukuu ya Pasaka.
29Hivyo Pilato akatoka nje walikokuwa akawauliza, “Mmeleta mashtaka gani kumhusu mtu huyu?”

30Wao wakamjibu, “Kama huyu mtu hakuwa mhalifu tusingemleta kwako.”

31Pilato akawaambia, “Basi mchukueni ninyi mkamhukumu kwa kufuata sheria zenu.”

Wayahudi wakamjibu, “Sisi haturuhusiwi kutoa hukumu ya kifo kwa mtu yeyote.”
32 cWalisema hivyo ili yale maneno aliyosema Yesu kuhusu kifo atakachokufa yapate kutimia.

33 dKwa hiyo Pilato akaingia ndani ya jumba la kifalme, akamwita Yesu, akamuuliza, “Wewe ndiye mfalme wa Wayahudi?”

34 eYesu akamjibu, “Je, unauliza swali hili kutokana na mawazo yako mwenyewe, au uliambiwa na watu kunihusu mimi?”

35 fPilato akamjibu, “Mimi si Myahudi, ama sivyo? Taifa lako mwenyewe na viongozi wa makuhani wamekukabidhi kwangu. Umefanya kosa gani?”

36 gYesu akajibu, “Ufalme wangu si wa ulimwengu huu. Ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, wafuasi wangu wangenipigania ili nisitiwe mikononi mwa Wayahudi. Lakini kama ilivyo, ufalme wangu hautoki hapa ulimwenguni.”

37 hPilato akamuuliza, “Kwa hiyo wewe ni mfalme?” Yesu akajibu, “Wewe wasema kwamba mimi ni mfalme. Kwa kusudi hili nilizaliwa, na kwa ajili ya hili nilikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Mtu yeyote aliye wa kweli husikia sauti yangu.”

38 iPilato akamuuliza Yesu, “Kweli ni nini?” Baada ya kusema haya Pilato akaenda nje tena akawaambia wale viongozi wa Wayahudi waliomshtaki Yesu, “Sioni kosa lolote alilotenda mtu huyu.
Copyright information for SwhNEN